RSS

Tag Archives: Bajeti ya Tanzania

Baadhi Ya Wabunge Watetea Ukuaji Deni La Taifa

Dodoma, Tanzania
 
 
 
BAADHI Ya Wabunge wa Bunge la Tanzania wametetea ukuaji wa deni la taifa.

Wabunge wamesema mjini Dodoma kuwa, deni hilo halihatarishi  hali ya nchi na hakuna nchi isiyokopa.
 
 
  Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina (CCM), amesisitiza kutoiunga mkono Bajeti ya Serikali, lakini amelitaka Bunge
 
limsaidie Rais Jakaya Kikwete, kwa alichodai pengine wasaidizi wake wameshindwa kumsaidia.
 
 

Mbali ya hilo, baadhi ya wabunge wamependekeza kuanzishwa kwa Wakala wa Barabara Vijijini kwa nia ya kuimarisha mtandao wa barabara za vijijini.
 

 
Wabunge walikuwa wakichangia hotuba za Mipango na Hali ya Uchumi pamoja na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2012/13, ikiwa ni siku ya tatu ya majadiliano baada ya kuwasilishwa hotuba hizo wiki iliyopita.
 
 

Mbunge wa Namtumbo, Vita Kawawa (CCM), alizungumzia kwa kirefu deni la taifa, na kuwaeleza wabunge
 
wenzake na Watanzania kwa ujumla kuwa deni hilo si kubwa kama baadhi ya watu wanavyoelezea.
 

 
“Huwezi kuzungumzia deni la taifa bila kuzungumzia Pato la Taifa. Lakini kwa kifupi, hali yetu ni nzuri. Deni letu ni
 

asilimia 54 ya Pato la Taifa wakati Japan ni asilimia 205 na Marekani 108.
 
 

“Deni tunalolipa kila mwaka ni asilimia tano ya mapato ya ndani, wakati kimataifa inatakiwa iwe asilimia 35, kwa hiyo, sisi
 
tuko pazuri. Ni vyema tukawaelimisha watu vizuri. Sisi hatuna mzigo mkubwa,” alisema Vita ambaye awali aliipongeza Serikali kwa kuboresha barabara za Mkoa wa Ruvuma.
 
 

  Mbunge wa Meatu, Meshack Opulukwa (Chadema) amesema, kukopa si kitu kibaya, ila Serikali inapaswa kulipa madeni yakiwamo ya ndani kama ya walimu.
 

 
Mpina ambaye alishatangaza kuwa hataiunga mkono Bajeti ya Serikali, jana katika mchango wake, alithibitisha hilo na akasema anafanya hivyo kwa sababu Serikali imeshindwa kutekeleza iliyoyaahidi mwaka uliopita.
 

 
Alizitaja sababu kuwa ni pamoja na kutoelezwa fedha zilizotengwa katika mwaka wa fedha unaomalizika zimetumikaje; kutopewa majibu na Serikali kuhusu hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na umbile la Bajeti sio sahihi kwa kutozingatia Mpango wa Maendeleo wa Taifa.
 
 
“Serikali imevunja sheria, kwa hali yoyote ingeweza kupelekwa mahakamani. Bunge ni lazima liwe na uhakika fedha za umma zinakwenda wapi? Bunge hili limsaidie Rais, kwani wasaidizi wake wanaonekana kushindwa,” alisema Mpina.
 
 
Mbunge wa Ukerewe, Salvatory Machemli (Chadema), alipendekeza kufufuliwa kwa viwanda, akisema bila kuzalisha, taifa haliwezi kuendelea; na pia kutaka wavuvi wasaidiwe baada ya bei ya sangara kushuka.

Posted by MJ

About these ads
 
Leave a comment

Posted by on June 21, 2012 in Tanzania News

 

Tags: , , , , ,

Kutoka Bungeni : Zitto on Government Budget

MFblog Inaendelea kuleta matukio yanayoendelea Mjini Dodoma katika kipindi hiki cha kikao cha Bunge cha bajeti. “ALL EYES ON DODOMA-BUNGENI”

Mh. Zitto Kabwe

Mh. Zitto Kabwe

WAZIRI Kivuli wa Fedha Kabwe Zitto amewasilisha bungeni bajeti mbadala ya Kambi ya Upinzani kwa mwaka wa fedha 2012/2013.
Zitto amebainisha kasoro nyingi zilizopo katika bajeti ya Serikali iliyowasilishwa bungeni Alhamisi iliyopita.
Bajeti ya Zitto ilitanguliwa na hotuba ya Msemaji  Mkuu wa Kambi ya Upinzani kuhusu Ofisi ya Rais – Mipango, Christina  Mughwai ambaye pia alibainisha alichokiita udhaifu wa Serikali  katika kuitekeleza mipango yake ya kiuchumi.
Zitto ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni katika hotuba yake  alisema mapato ya Serikali yanaweza kuongezwa kwa Sh2.885 trilioni,  hivyo kupunguza utegemezi wa mikopo ya kibiashara ambayo imekuwa  ikiligharimu taifa kiasi kikubwa cha fedha. Vyanzo vya kodi na  kiasi cha fedha kwenye mabano alivyopendekeza ni marekebisho ya kodi za  misitu ukiwemo mkaa (Sh130.8 bilioni), kupunguza misamaha ya kodi,  kuzuia ukwepaji kodi na udanganyifu wa biashara ya nje (Sh742.74  bilioni), mauzo ya hisa za Serikali (Sh415.55 bilioni), Marekebisho ya  kodi Sekta ya Madini na asilimia 25 ya Mauzo ya Madini Nje (Sh578.36  bilioni) na Marekebisho ya Kodi na Usimamizi bora wa Mapato Kampuni za  Simu (Sh502.26 bilioni).

Mapendekezo mengine ni Marekebisho ya  Kodi ya Tozo ya Kuendeleza Stadi (Sh243.52 bilioni), mapato ya  wanyamapori (Sh61.64 bilioni), kuondoa msamaha wa ushuru wa mafuta kwa  kampuni za madini (Sh44.9 bilioni), Usimamizi wa mapato ya utalii  (Sh51.75 bilioni), Kuimarisha biashara Afrika Mashariki (Sh 114.15  bilioni).

Zitto alisema kama wapinzani wangekuwa madarakani  wangekusanya kiasi cha Sh15 bilioni sawa na ile ya Serikali, lakini  tofauti ni hatua ya kutenga asilimia 35 ya mapato ya ndani kwa ajili ya  utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kupunguza utegemezi wa bajeti  kutoka asilimia 42.37 za Serikali hadi asilimia 21.3.

 

Amesema, Serikali haipaswi kuendelea kukopa, kwani taarifa rasmi za kibenki na  ukaguzi wa hesabu zinaonyesha kwamba deni hilo linakua kwa kasi tofauti  na maelezo ya Serikali kwamba linahimilika.

“Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali inaonyesha kuwa Deni la Taifa  linazidi kuongezeka kwa asilimia 38 kutoka Sh10.5 trilioni mwaka  2009/2010 hadi Sh14.4 trilioni 2010/2011. Kwa mujibu wa Waziri wa Fedha, Deni la Taifa limefikia Sh20.3 trilioni mpaka ilipofika mwezi Machi  mwaka 2012,”

alisema Zitto na kuongeza:       “Ukisoma taarifa ya Mwezi wa Mei 2012 ya Benki Kuu ya Tanzania, Deni la Taifa sasa limefikia Sh22 trillion. Suala hapa sio ustahmilivu wa Deni kama inavyodai Serikali,  bali ni kwamba tunakopa kufanyia nini?”

Alisema hesabu za bajeti ya Serikali ya 2012/13 inayopendekezwa zinaonyesha kwamba Serikali bado ina mpango wa kukopa kwa ajili ya kugharamia matumizi ya kawaida ambayo hayazalishi wala kutozwa kodi. “Hatutaki mikopo kwa ajili ya  matumizi ya kawaida ya posho, kusafiri, magari n.k. Tuchukue mikopo  kuwekeza kwenye miradi itakayokuza uchumi na kuzalisha kodi zaidi,”  alisema.

Kuhusu mfumuko wa bei, Zitto alikosoa hatua  zinazopendekezwa na Serikali kukabiliana nao, kwamba ni zile  zilizoshindwa katika mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, mwaka huu. Alisema hatua hizo ambazo ni kutoa vibali kwa wafanyabiashara vya kuagiza  mchele na sukari bila kutoza kodi, haziwezi kusaidia kwa kuwa hatua kama hizo zilipochukuliwa awali zilisababisha bei ya bidhaa hizo kuongezeka. “Baada ya hatua hii bei ya sukari ilipanda kutoka Sh1,700 mpaka 2,800 kwenye  maeneo mengi nchini… Serikali inachukua hatua zile zile kwa tatizo lile  lile ikitegemea matokeo tofauti,” alisema Zitto.

Alirejea  pendekezo la mwaka jana kwa Serikali kutoa vivutio kwa wakulima wadogo  kuzalisha chakula kwa wingi akisema kuwa hatua hiyo pekee ndiyo  itapunguza mfumuko wa bei. “Hakuna mbadala wa kudhibiti mfumuko  wa bei zaidi ya kuongeza uzalishaji wa chakula na kuwekeza kwa wananchi  wetu.

Serikali inafikiria uzalishaji utaongezeka kwa kusaidia wakulima  wakubwa ambao watageuza wananchi wetu kuwa manamba na vibarua ndani ya  nchi yao,” alisema na kuongeza: “Tuwekeze kwa watu wetu vijijini ili waongeze uzalishaji na kwa kufanya hivyo mfumuko wa bei ya chakula  utakuwa historia. Hakuna mwarobaini wa kupanda kwa bei za vyakula  isipokuwa kilimo”.

MF: Well done Zitto; Tunaendelea Kufuatilia yanayoendelea Dodoma kwa Ukaribu.

 

 
3 Comments

Posted by on June 19, 2012 in Tanzania News

 

Tags: , , , , , , , ,

Kutoka Bungeni: Misamaha ya Kodi Kupunguzwa

Dodoma, Tanzania

 

WIZARA ya Fedha imesema, Serikali ina lengo la kupunguza misamaha ya kodi ili isizidi asilimia moja ya pato la taifa.

Naibu wa Fedha Ms.Saada Mkuya,Mb.

Naibu wa Fedha Ms.Saada Mkuya,Mb.

 

Naibu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum ameliambia Bunge mjini Dodoma kuwa, Serikali inaendelea kupitia baadhi ya sheria za misamaha ya kodi ili kuangalia kama bado zina manufaa kwa umma.

 

Amesema, ili kutimiza azma hiyo, Mamlaka ya Mapato (TRA) kupitia mfuko wa dhamana wa ushauri wa sera na usimamizi wa kodi ulioanzishwa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) inafanya uchambuzi wa kina wa kuangalia sheria na kanuni za misamaha ya kodi.

 

Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa Serikali, uchambuzi huo utaleta mapendekezo ya kuiondoa misamaha yote isiyo na maslahi na tija kwa taifa.

 

Salum amesema, mwaka ujao wa fedha, Serikali imechukua hatua za kurekebisha sheria mbalimbali za kodi kwa nia ya kupunguza misamaha na kuzuia mianya ya ukwepaji kodi.

 

Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu Amina Abdulla Amour (CUF) aliyetaka kufahamu ni lini Serikali itapunguza misamaha yakodi hadi kufikia chini ya asilimia moja ya pato la taifa kutokana na kuwa kero kwa muda mrefu kwa taifa kukosa fedha na mapato kwa ajili ya maendeleo.

 

“Sisi pale wizarani tumeamua kulivalia njuga suala hili, tutaifanya kazi hiyo na tunaomba tupewe muda kwani jambo hili haliwezi kufanyika kwa mara moja,” alisema.

 

Wakati huo huo, Salum alisema Benki ya Wanawake inaweza kushiriki katika mpango wa kukopesha na kusimamia fedha za mabilioni ya Rais endapo inahitaji kufanya hivyo na taasisi zingine za fedha ambazo zimekidhi vigezo vilivyowekwa.

 

Alitaja vigezo hivyo kuwa ni pamoja na uwezo wa kuhudumia vijijini, kuwa na mizani nzuri za hesabu na uzoefu katika kuhudumia wajasiriamali wadogo.

 

Alisisitiza kuwa walengwa wa mfuko wa mabilioni ya Rais ni vijana, wazee, wanawake vijijini na mijini ambao wanafanya shughuli katika kuhudumia wajasiriamali wadogo.

 

Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu Faida Mohamed Bakar (CUF) ambaye alihoji kama Serikali inakubaliana naye kwamba sasa ni wakati muafaka wa kuhamisha fedha za mkopo wa mabilioni ya Kikwete na kutumika katika Benki ya Wanawake ili wananchi wapate mikopo.

 

Wakati huohuo, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Fedha na Uchumi, imeafiki maeneo mengi ya kodi na tozo mbalimbali yaliyopendekezwa na Serikali kufanyiwa marekebisho, lakini ikasisitiza umuhimu wa nidhamu ya matumizi ya Serikali na uwezo wa kuongeza mapato.

 

Mbali na hayo, Kamati hiyo ilieleza kutoridhishwa na Serikali katika kasi ya kushughulikia misamaha ya kodi.

 

“Kamati inaishauri Serikali kuonesha dhamira ya kweli kufanikisha lengo hilo (la kuimarisha taratibu za kukusanya mapato pamoja na kupunguza misamaha ya kodi) na kutoa taarifa ya utekelezaji mbele ya Kamati Januari 2013,” amesema Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Andrew Chenge.

 

Chenge alikuwa anawasilisha taarifa ya Kamati yake kuhusu hali ya uchumi wa Taifa kwa mwaka 2011 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2012/13 pamoja na tathimini ya utekelezaji wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2011/12 na mapendekezo ya mapato na matumizi ya Serikali kwa 2012/13.

 

“Kamati inaendelea kushauri kwamba Serikali iachane na mtindo wa kuibua matumizi mapya yasiyo ya dharura ambayo hayakuidhinishwa na Bunge wakati wa utekelezaji wa bajeti”

 

“Mtindo huo unavuruga bajeti na kupunguza uwezo wa kutoa fedha za matumizi mengineyo (OC) na matumizi ya maendeleo kama ilivyokusudiwa. Kamati inasisitiza umuhimu wa Serikali kubana matumizi kwa kupunguza matumizi yasiyo ya lazima,” amesema Chenge.

 
Leave a comment

Posted by on June 19, 2012 in Tanzania News

 

Tags: , , , , , , ,

Tanzania: Sekta binafsi walia na TRA

Dodoma, Tanzania.

 
TAASISI ya Sekta binafsi nchini (TPSF) imesema, uwezo mdogo wa kukusanya kodi wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) unasababisha bajeti kuegemea kuongeza kodi kwenye bidhaa za vinywaji ambavyo vinaaminika kuwa ni chanzo cha mapato yao.
 
Pia taasisi hiyo imeshauri Serikali ianzishe utaratibu wa kuajiri kwa mikataba ya miaka mitatu tu ili kuweza kuwa na nidhamu katika utendaji kazi na matumizi ya fedha za umma pia.
 
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa  TPSF, Godfyey Simbeye wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa juu ya kauli ya taasisi hiyo baada ya Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa kuwasilisha bajeti ya Serikali jana.
 
Alisema, hii inaonesha dhahiri kuwa TRA haina orodha kamili ya walipa kodi  ambao hali ambayo kwa kiasi kikubwa ndiko kiasi kikubwa cha mapato kinakopotea na hivyo kujikuta wakilazimika kukandamiza kodi kubwa katika vinywaji.
 
Alisema kuwa, uamuzi huu wa kuongeza bajeti katika vinywaji haujafanyika katika bajeti hii ya 2012/2013 bali inafanyika karibu bajeti zote katika kila mwaka.
 
“Wenzetu wa nchi ya Kenya, katika bajeti yao ya mwaka jana hawakugusa kabisa kupandisha kodi katika vinywaji, inaonesha wanakusanya kodi yao katika maeneo mengine,” alisema Mkurugenzi huyo.
 
Aidha aliongeza kuwa, ni jambo la kushangaza pale ambapo Wabunge walishangilia baada ya kusikia Waziri wa Fedha na Uchumi, alipotangaza kuongeza kodi katika sigara na bia kwa asilimia 25 ili kuweza kuwadhibiti walevi.
 
Alisema kuwa hivi sasa Tanzania ina watu milioni 45, lakini walipa kodi  ni watu 500 hali ambayo huchangia Serikali kushindwa kukusanya mapato stahiki na kuendelea kunyonya walipa kodi wadogo.
 
“Labda vitambulisho vya taifa vitasaidia nchi hii kuweza kukusanya kodi na kuacha kuangalia kwenye bia na soda,” alisema.
 
Pia alibainisha kuwa, kama sekta binafsi  haikupendekezwa na Serikali kutenga asilimia 70 kwenda kwenye matumizi ya kawaida huku asilimia 30 kwenda kwenye shughuli za maendeleo hali ambayo inaonesha kuwa hakutakuwa na ushindani kwenye biashara.
 
“Sekta binafsi inapendekeza angalau asilimia 65 ingetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida na kwenye shughuli za maendeleo iwe asilimia 35 ili kwenda sambamba na soko la pamoja la Afrika Mashariki,” alisema.
 
 Alisema kuwa, bajeti haikueleza kama Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) atawezaje kuzuia matumizi mabaya ya fedha za umma.
 
Simbeye alisema kuwa, suala la kuvutia uwekezaji linasuasua kutokana na kutokuwa na benki ya ardhi kwani hakuna ardhi inayotengwa kwa ajili ya uwekezaji katika kilimo.
 
“Serikali ifikirie kuwa na benki ya ardhi na wangeanza na mikoa mitano kama majaribio, suala la ardhi lingetengewa bajeti hilo pia lingerahisisha hata ukusanyaji wa kodi,” alisema.
 
Pia alitaka leseni isiwe chanzo cha kukusanya mapato kwenye Halmashauri na kuangaliwa kwa mikakati ya kukuza viwanda ambayo bado haijawekwa vizuri.
 
Aidha alisema kuwa bajeti ya mwaka huu haiwezi kubadilisha maisha ya Mtanzania kwa kiwango kilichotarajiwa kwani haikuongelea suala la bei ya mafuta.

Posted by MJ

 
Leave a comment

Posted by on June 19, 2012 in Tanzania News

 

Tags: , , , ,

Mbunge Wa CCM Kuipinga Bajeti

Dodoma, Tanzania – Mwandishi wa MF Blog

MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina (CCM) ameapa kuipinga bajeti ya Serikali iliyowasilishwa bungeni mjini Dodoma, kwa maelezo kwamba imejaa ulaji wa wakubwa kupitia posho, warsha na safari zao za nje huku mamilioni ya Watanzania masikini wakifa kwa kukosa matibabu.

Amewaeleza waandishi wa habari kuwa, bajeti hiyo inakiuka azimio la Bunge kwamba kwa kila mwaka wa fedha angalau asilimia 35 itengwe kwa ajili ya miradi ya maendeleo na fedha za matumizi ya kawaida ziwe asilimia 65.

Lakini Mpina ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi alisema bajeti iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa, waliipinga kuanzia kwenye Kamati ya Fedha na kuishauri Serikali iibomoe, lakini hawakufanya hivyo.

Mbunge huyo amesema, yuko tayari kufukuzwa CCM akitetea fedha zaidi zitengwe kwa ajili ya miradi ya maendeleo, kwani warsha, sherehe, ununuzi wa samani, magari ya kifahari unaweza kupunguzwa au kuahirishwa ili kuwapa Watanzania maisha bora.

“Hiki ninachofanya si usaliti kwa chama, kwani ninachotetea ni kukisaidia chama chetu kiweze kutekeleza miradi yenye manufaa kwa wananchi na si kutenga fedha nyingi kwa posho na sherehe,” alisema Mbunge huyo.

Akichambua bajeti hiyo, Mpina alisema katika azimio la Bunge iliazimiwa kitengwe kiasi kisichopungua Sh trilioni 2.7 kutoka mapato ya ndani na zielekezwe kutekeleza mpango huo.

“Hivyo bajeti ambayo imewasilishwa na waziri si sahihi kwa mujibu wa mpango wa maelekezo ya Bunge,” alisema.

Akitoa mfano wa ulaji huo, Mbunge huyo alisema mafungu nane tu ya Wizara ya Nishati na Madini na  Fedha yameongezwa kiasi cha Sh bilioni 4.8 kwa ajili ya posho na safari za ndani na nje ya nchi, wakati fedha hizo zingepunguzwa na kuelekezwa kwenye miradi ya maendeleo.

Alisisitiza kuwa kitendo cha Serikali kutenga Sh trilioni 2.2 badala ya Sh trilioni 2.7 ambayo ni tofauti ya Sh bilioni 500 kugharimia miradi iliyoainishwa katika mpango huo,  kumesababisha miradi mingi kutengewa fedha kidogo na mingine mingi kukosa fedha kabisa, hali ambayo alidai inazorotesha utekelezaji na maana ya kuwa na mpango.

Mpina alisema kibaya zaidi, katika bajeti hiyo mapato ya ndani yameongezeka hadi Sh trilioni 1.5 huku matumizi ya kawaida yakipanda hadi Sh trilioni 1.9 wakati fedha za maendeleo zikipungua na kuwa Sh bilioni 397.8 ikilinganishwa na mwaka wa fedha wa 2011/12.

“Hapa inajidhihirisha kuwa Serikali haina nia ya dhati ya kupunguza matumizi ya kawaida,” alisema Mpina. Alisema kwa kipindi kirefu, imekuwa ikiahidi kupunguza matumizi ya kawaida ili kuongeza kasi ya utoaji huduma na uwekezaji katika sekta zinazokuza uchumi na kupunguza umasikini; lakini hivi sasa pato kuu la Taifa linatumika kuendesha Serikali.

Mpina alisema wakati Serikali ikiendekeza matumizi makubwa yasiyo na tija, Watanzania wanakufa kwa kukosa huduma za tiba, dawa, waganga, maji safi na salama, elimu bora kutokana na upungufu mkubwa wa madarasa, nyumba za walimu, vifaa vya kufundishia na maabara.

Pia miundombinu mibovu ya barabara, umeme na reli, ukosefu wa viwanda vya kuongeza thamani kunakosababisha wakulima kuuza mazao yao kwa bei ndogo, hasa pamba, mkonge, korosho na mifugo.

Alisema mpango wa maendeleo ni mkataba kati ya wananchi na Serikali, lazima wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi waulinde kwa nguvu zote na kwa gharama yoyote.

Alisema kama Serikali ilipata fedha za kufidia benki na wafanyabiashara walioathirika na mtikisiko wa uchumi kwa jumla ya Sh trilioni 1.7 “iweje leo ishindwe kupata Sh bilioni 500 kugharimia yaliyoainishwa katika mpango wa maendeleo?”

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Fedha na Uchumi, Andrew Chenge alisema ingawa Waziri wa Fedha ameanza kwa mwelekeo mzuri, lakini matumizi ya kawaida ya Serikali yanapaswa kugharimiwa na fedha za ndani.

Mbali ya kusisitiza bajeti ya maendeleo iongezwe hadi asilimia 35, amesema kama Watanzania wanataka uchumi ukue na kuondoka na umasikini, lazima kilimo kibadilishwe na kiwe chenye tija.

“Mwelekeo mzuri, wameanza vizuri,” alisema Chenge ambaye pia ni Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM) aliyepata kuwa Waziri katika Awamu ya Nne.

Mwenyekiti huyo aliyechaguliwa hivi karibuni kuongoza Kamati hiyo ya Bunge, alisema licha ya kuanza vyema yapo mambo ambayo hayakumridhisha katika bajeti.

“Lazima tufanye matumizi ya kawaida kwa kutumia mapato ya ndani. Hili tulilizungumza katika Kamati yetu wakati wa mashauriano na Serikali. Lakini tulisema kwa kuwa Waziri ni mgeni, ndio kwanza ameteuliwa, tumpe muda, ajipange hadi bajeti ya 2013/14,” alisema Chenge.

Alisema ni vyema pia sekta binafsi ikawekewa mazingira mazuri ili kushawishi ukuaji wa uchumi; huku akieleza kwamba tayari kampuni za bia na sigara zimeeleza kusikitishwa na ongezeko la bei katika bidhaa zao.

Kuhusu kilimo, alisema lazima Serikali isaidie kuweka miundombinu bora ya kilimo na kuhakikisha barabara zinapitika wakati wote ili wakulima waweze kutoa mazao yao mashambani na kuyapeleka sokoni.

Alisema si hivyo tu, bajeti inapaswa kulenga watu wa vijijini ambako ndiko waliko asilimia kubwa ambao ni wakulima, ili kuzalisha kwa wingi na kuiwezesha nchi kuwa na uchumi imara.

Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka (CCM), alisema baadhi ya maeneo, Serikali haijafanya vizuri katika bajeti ikiwamo kutoa nafuu ya kodi kwa kampuni kubwa zikiwamo za madini.

Alisema unafuu huo wa kodi haufai kwa kampuni na viwanda vikubwa, wakati wanapaswa kulipa kodi kubwa.

Aidha, Sendeka alilalamikia kiwango kidogo kilichotengwa kwa umeme, Sh bilioni 400, akisema hazitoshelezi kwa sababu ya gharama kubwa za kukodi mitambo ya kuzalisha umeme zinazobebwa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, alitaka Serikali itaje kiasi cha mishahara kilichoongezwa, badala ya kuachiwa waziri wa kisekta, kwa sababu hilo ni moja ya maeneo yanayohitaji uzito.

Aidha, alilalamikia matumizi kuwa makubwa, kutofutwa kwa posho, mfumuko wa bei akisema umejikita katika kuagiza chakula nje na kuanzisha kilimo cha umwagiliaji katika mabonde makubwa nchini.

Mbunge wa Kigoma Kaskazini ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni,  Kabwe Zitto alisema bajeti hiyo imejikita zaidi katika mikopo na madeni.

Katika hotuba yake ya Bajeti, Dk Mgimwa alisema katika bajeti hiyo yenye kubeba Sh trilioni 15, asilimia 70 itakuwa kwa matumizi ya kawaida na asilimia 30 kwa matumizi ya maendeleo.

Wakati hayo yakijiri, wabunge wa CCM walikuwa na kikao jana asubuhi; na miongoni mwao walieleza kutoridhishwa ni kutofutwa kwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika malighafi za viwanda vya nguo na mavazi.

Mmoja wa wabunge hao wa CCM, alieleza kuwa licha ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuunda kamati maalumu ya wadau wa sekta ya pamba na viwanda vyake, mapendekezo ya kamati hiyo hakuyazingatiwa katika bajeti.

Mapendekezo yalikuwa ni viwanda kupewa msamaha wa VAT kwenye bidhaa za nguo na mavazi, na ilielezwa kuwa hilo linawezekana kwa sababu kiwango kinachokusanywa sasa ni karibu Sh bilioni moja kwa mwaka.

 
Leave a comment

Posted by on June 17, 2012 in Tanzania News

 

Tags: , , , , , ,

 
Follow

Get every new post delivered to your Inbox.

Join 3,835 other followers