BENKI ya Afrika Tanzania imeongeza faida yake mara mbili kufikia nusu ya mwaka huu 2012 kulinganisha na kipindi hicho kwa mwaka 2011.
Taarifa ya fedha iliyotolewa hivi karibuni, ilieleza kuwa benki hiyo imepata Sh milioni 551 katika robo ya mwaka inayoishia Juni 2012 kulinganisha na Sh milioni 273 iliyopata katika kipindi hicho mwaka jana.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Idara ya Fedha wa benki hiyo, Mussa Mwachaga, faida iliyopatikana kutokana na riba ni Sh bilioni nne katika robo ya mwaka inayoishia Juni 2012 kulinganisha na Sh bilioni tatu iliyorekodiwa katika kipindi hicho mwaka jana.
Mwachaga alisema benki imerekodi faida inayotokana na riba ya Sh bilioni 8.2 katika kipindi kinachoishia Juni mwaka huu ukilinganisha na Sh bilioni 5.7 zilizorekodiwa katika kipindi kama hicho mwaka jana.
Benki ya Afrika Tanzania imekuwa ikijitahidi kujitanua na kuimarisha huduma zake katika miaka ya hivi karibuni.
Tangu ianzishwe nchini mwaka 2007, imeshafungua matawi 10 mkoani Dar es Salaam na sita nje ya mkoa huo yakiwamo ya Morogoro, Tunduma, Mwanza, Moshi, Mbeya and Arusha.
Benki hii ni moja ya mtandao wa kibenki unaofanya kazi katika nchi 15 ambazo ni Benin, Burkina Faso, Ghana, Ivory Coast, Mali, Niger, Senegal, Burundi, Djibouti, Kenya, Madagascar, Tanzania na Uganda. Pia ina tawi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.