RSS

Daily Archives: July 11, 2012

Kilo 700 za kahawa toka Kigoma zakataliwa sokoni‏

KIGOMA

ZAIDI ya kilo 700 za kahawa zilizopelekwa kwenye Mnada wa Kimataifa wa Kahawa Moshi mkoani Kilimanjaro kutoka Kigoma, zimekataliwa na kurudishwa kwa wenyewe kwa madai kuwa hazina ubora kati ya madaraja 11 ya ubora wa kahawa yanayotambulika nchini.

Meneja wa Chama Kikuu cha Wakulima wa Kahawa mkoani Kigoma (KANYOVU), Jeremia Nkangaza alisema hayo wakati akitoa taarifa ya utekelezaji ya chama hicho kwa mwaka uliopita katika mkutano mkuu wa mwaka wa chama hicho.

Nkangaza alisema kuwa kahawa hiyo iliyorudishwa, inatoka kwa wakulima ambao wamekuwa wakifanyia shughuli zao za utayarishaji kahawa nyumbani na kilichogundulika  ni kwamba wakulima waliichemsha ili iwahi kuiva na kuiwahisha sokoni.

Alisema uboreshaji wa kahawa imekuwa changamoto kubwa kwao kama chama na wakulima, jambo ambalo limechangia kushusha bei ya kahawa ambayo imekuwa ikitayarishwa nyumbani kwa vile wakulima wengi hawafuati kanuni 10 za utayarishaji wa zao hilo.

Hata hivyo kwa mujibu wa Nkangaza, kumekuwa na mafanikio makubwa kwa kahawa inayotayarishwa katika vituo maalumu kutokana na kufikia ubora wa juu na kufanikiwa kuuza kilo moja kwa kati ya Sh 8,000 hadi 8,500.

Alisema kwa msimu uliomalizika, kilo 294,081 za kahawa safi iliyozalishwa vituoni iliuzwa kwa bei hiyo ambapo kati ya hizo, kilo 192,000 ziliuzwa katika soko la moja kwa moja.

Meneja huyo alisema kilo 658, 608 zilizotayarishwa nyumbani zilikusanywa na katika mnada uliofanyika Moshi mkoani Kilimanjaro kila kilo iliuzwa kwa Sh 596 ikiwa na tofauti kubwa ya bei kati ya ile inayotayarishwa kwenye vituo.

Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Chama cha Msingi cha Rumako, Yahaya Mahwisa alisema ipo haja ya maazimio yaliyofikiwa kwenye mkutano wa wadau yakatekelezwa kwa wakulima kubanwa ili watayarishe kahawa yao kwenye vituo na kuifanya kuwa na ubora na kupata soko la uhakika.

Mahwisa alisema kahawa inayozalishwa mkoani Kigoma imekuwa ikipendwa sana katika soko la dunia kutokana na muonjo wake lakini kumekuwa na kiasi

kidogo kinachozalishwa kwa ubora wa juu ambao wanunuzi wa maja kwa moja wanaitaka na hivyo kuwakatisha tamaa wanunuzi kupata kiasi cha kutosha.

Mwenyekiti wa Kanyovu, Mathias Dangwa alisema vyama vya wakulima wa kahawa mkoani Kigoma haviungi mkono kitendo cha kushawishi wakulima wauze kahawa mbivu kama sera ya soko huria inavyotaka kutokana na utaratibu huo kuchangia wizi wa kahawa mashambani.

Dangwa alisema utaratibu huo unapingana na mkakati wa uboreshaji wa kahawa katika kupata ubora wa juu kwani ni jambo gumu kusimamia ubora kwa kahawa ambayo inauzwa moja kwa moja kwa mnunuzi kutoka shambani badala ya kupitia kwenye vituo vya uboreshaji au kwenye chama.

 

About these ads
 
Leave a comment

Posted by on July 11, 2012 in Tanzania News

 

Tags: , , , ,

ATCL yarejesha safari za Comoro‏

KAMPUNI ya Ndege ya Tanzania (ATCL) imerejesha safari ya kutoka Dar es Salaam kwenda Hahaya katika visiwa vya Comoro, ikitekeleza mpango wa miaka mitano wa kuongeza idadi ya ndege na safari zake.

Akizungumza baada ya kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Prince Said Ibrahim mjini Hahaya jana, Kaimu Mkurugenzi wa Biashara wa ATCL, Mwanamvua Ngocho alisema, kampuni hiyo itakuwa ikifanya safari zake mara nne kwa wiki katika njia hiyo. ATCL ilifuta safari zake za Dar es Salaam – Hahaya mwaka 2008.

“Tumezindua upya safari yetu ya Dar es Salaam – Hahaya (Comoro) ikiwa ni safari yetu ya kwanza ya kimataifa tangu tuliporejesha utoaji wa huduma miezi miwili iliyopita. Tumeamua kuizindua upya safari hii ili kuitumia vilivyo ndege yetu ya Boeing 700-500 ambayo ilikuwa haina kazi baada ya kumaliza safari ya Dar- es Salaam-Mwanza-Kilimanjaro asubuhi,” alisema Ngocho na kuongeza:

“Tumeamua kuchagua njia hii kutokana na umuhimu wake kiuchumi nchini. Tuna imani kuwa jitihada zetu zitasaidia kuongeza mahusiano mazuri baina ya nchi hizi mbili na vilevile kutoa nafasi kwa abiria kutoka Comoro kusafiri sehemu mbalimbali kupitia Dar es Salaam.”

Alisema, kampuni hiyo bado ina mpango wa kujikita katika kuongeza safari za ndani na nje ya nchi, akizitaja safari hizo kuwa ni Dar es Salaam – Lusaka (Zambia), Dar es Salaam – Johannesburg (Afrika Kusini) na kusisitiza mipango hiyo itakamilika endapo watapata ndege nyingine katika muda mfupi ujao.

“Tayari tuko katika mazungumzo ya kupata ndege nyingine ambayo itatusaidia kujikita katika safari za kimataifa. Katika mpango huo, tutashirikiana kibiashara na baadhi ya kampuni za ndege ili kuweza kulifanikisha hili,” alisema Kaimu Mkurugenzi huyo.

“Bidhaa nyingi zitumikazo nchini Comoro zinatokea Tanzania. Wananchi wanatakiwa kuitumia fursa hii ipasavyo kutokana na ukweli kwamba ATCL itatoa huduma ya usafirishaji kwa bei nafuu,” alisema.

 
Leave a comment

Posted by on July 11, 2012 in Tanzania News

 

Tags: , , , , , ,

 
Follow

Get every new post delivered to your Inbox.

Join 3,835 other followers

%d bloggers like this: